NGUVU KUBWA NYUMA YA IMANI

Shalom, na Karibu katika kile ambacho nimeona vyema tushirikishane kidogo, Leo hii kwa ufupi kidogo hebu tujaribu kuangazia suala la Imani na Nini umuhimu wake Kwa Mwanadamu(Mwamini). Biblia katika Kitabu Cha Waebrania 11: 1 inatuambia hivi "Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana." Kutoka katika Mstari huo tunaona mambo makubwa mawili kuhusu Imani, kwanza ni "uhakika wa mambo yanayotarajiwa" sijajua upande wako, lakini Mimi naona Jambo kubwa sana hapa, kinachokuja kwenye ufahamu wangu ni hiki; Kawaida watu huwa hawana uhakika na mambo wanayoyatarajia lakini suluhisho la Jambo hilo ni kuwa na Imani, ukiwa nayo hii, tayari unauhakika wa hayo. Biblia ya Kiingereza toleo la KJV inaita huo uhakika "Substance" yaani ndio Kitu chenyewe. Jambo jingine katika Mstari huo ni "Bayana ya mambo yasiyoonekana" Neno "Bayana" maana yake ni wazi, au ushahidi wa uhalisia, KJV inaitwa Kwa Kiingereza "Evidence" NIV inaita "assurance" Sasa mambo yaha mawili yakiwa Kwa Mwamini unaona Kabisa kwamba yatakuwa ni suluhisho la mambo mengi sana kwake, Amani yake, Furaha yake, tumaini lake Kwa Bwana na mengine Mengi, nafikiri labda hakuna jambo jingine katika maisha ya Kikristo ambalo ni muhimu zaidi kuliko imani. Kwa bahati mbaya, hatuwezi kununua, kuuza, au kuazima Kwa marafiki zetu. Hii tunaipokea Kwa Mungu na kuanza kuifanyia kazi ili iendelee kukaa kwetu na Kukua, pengine umewahi kusikia Maneno haya(Roho ya Imani, Mbegu ya Imani, kipawa/karma ya Imani) mambo hayo na mengine kadhaa huwa wakati fulani yanatumika kuonyesha aina za Imani ambazo mtu anaweza kukirimiwa, ila Kwa upana wake tutajifunza wakati Mwingine, Leo tuendelee kidogo na Msingi hasa.

Sasa Imani sio tu ni muhimu Kwa Mwamini katika hayo niliyoyataja hapo Juu, bali pia, ili Mwamini awe na uhusiano na Mungu lazima awe na Imani, Katika sure hiyohiyo ya Kitabu Cha Waebrania Mstari wa 6 Biblia inasema "Lakini pasipo Imani, haiwezekani kumpendeza; Kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba Yeye yuko na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao" Kuna Neno limejitokeza kwenye huu Mstari linaitwa LAZIMA, Kama wewe ni Mwombaji, Umeokoka, unafanya kazi ya Mungu, unahitaji kumtwika Yesu mizigo yako, unahitaji kupata neema zaidi Toka kwake, basi LAZIMA, unapomwendea uamini kwamba Yeye yupo, na kwamba Kila ukimwendea hakuachi bure, anakupa thawabu, haleluya!

Tunaona mfano kamili wa hili katika Luka 7:50. Yesu anahusika katika majadiliano na mwanamke mwenye dhambi wakati anatoa maelezo ni kwa nini imani ni muhimu sana. "Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani." Mwanamke aliamini kwa Yesu Kristo kwa imani na akampa thawabu kwa ajili yake. Hatimaye, imani ni chombo kinachotuwezesha hadi mwisho, kwa kujua kwa imani kwamba tutakuwa pamoja na Mungu milele. " Biblia inasema hivi, 1Petro 1:8-9 "Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu, katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu"

Mifano ya imani. Waebrania sura ya 11 inajulikana kama "sura ya imani" kwa sababu ndani yake matendo makuu ya imani yanaelezwa. Kwa imani Abeli alitoa sadaka ya kupendeza kwa Bwana (mstari wa 4); Kwa imani Nuhu alijenga safina wakati ambapo mvua haijulikani Kama itanyesha lini (mstari wa 7); Kwa imani Ibrahimu alitoka nyumbani kwake na kutii amri ya Mungu ya kwenda Mahali ambako hajakufahamu Bado, kwa hiari alimtolea mwanawe pekee (mstari wa 8-10, 17); Kwa imani Musa aliwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri (mstari wa 23-29); Kwa imani Rahabu alipokea wapelelezi wa Israeli na akaokoa maisha yake (mstari wa 31). Mashujaa wengi wa imani wanatajwa "ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni."(mstari wa 33-34.)

Imani ni jiwe kuu la Ukristo. Bila kuonyesha imani na uaminifu kwa Mungu hatuna mahali pamoja naye. Tunajua kwamba Mungu yupo kwa imani. Imani inaweza kushindwa wakati mwingine, lakini kwa sababu ni zawadi ya Mungu, iliyotolewa kwa watoto Wake, hutolewa nyakati za majaribu na mateso ili kuthibitisha kuwa imani yetu ni halisi na kutuimarisha na kutujenga. Ndiyo maana Yakobo anatuambia tuchukulie kuwa ni "furaha" kwa sababu kujaribiwa kwa imani yetu, huku huleta uvumilivu na kukua, kutoa ushahidi kwamba imani yetu ni halisi (Yakobo 1: 2-4). Mungu akubariki, endelea kumwamini yeye, bado ana mengi sana Kwa ajili yako Kwa Wakati unaokuja. Amina!

By Robin Mwenda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *