NGUVU YA NEEMA(SEHEMU YA PILI)

Nakusalimu katika Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Na karibu katika mwendelezo wa somo letu!

Sasa sehemu iliyopita tuliishia katika kuona kwanini Torati iliingia na tukaona sababu ya kwanza, ni; Ili kuwaonyesha watu makosa yao na pia kuwafundisha kwamba lazima waishi kwa utaratibu. Pili, tuliona ni ili kuonyesha utangulizi wa uhalisia ambao ungekuja kwa njia ya Yesu Kristo au kwa lugha nyingine Torati ilikuwa ni kivuli. Na Sasa leo naomba tuanzie na kuona sababu ya tatu ambayo ni;

Torati ililetwa ili kuwa Kiongozi kutuleta mpaka ujio wa Yesu Kristo. Biblia inasema hivi; Galatia 3;23-25 " Lakini kabla ya kuja ile Imani tulikuwa tumewekwa chini ya Sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa ni Kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi." Sasa hili ni moja ya kazi kubwa Sana ambayo ilibebeshwa ndani ya torati. Ilikuwa inahakikisha inafanya kazi yake mpaka mwisho, na mwisho wake ni ujio wa Yesu Kristo. Ndio maana Yesu alipokuja alisema hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza (Mathayo 5; 17). Na Sasa basi, hapa Kuna jambo kubwa Sana la kuzingatia, Biblia inaendelea kuwa na agano la kale mpaka Sasa ili kutusaidia sisi kuelewa hata Yesu tunayemwamini na kumpenda ametoka wapi. Yesu Kristo anaanza kutajwa tangu kitabu cha Mwanzo na vingine vingi Sana katika agano la kale. Ila hiyo haifanyi Mambo yote ambayo torati imeagiza basi na sisi tuyafanye la hasha! Hebu fikiria kwa Sasa mtu akisema anatarajia dhambi zake zitakaswe kwa damu ya Mbuzi au Kondoo, bila shaka hataeleweka hata kidogo, kwanini? Kwasababu Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu yaani Yesu amekwisha kutolewa (Yohana 1;29) na kwa damu yake tunahesabiwaa haki bure. (Warumi 3:23-24). Pia ukiendelea kufuata kila kitu ambacho agano la kale limeagiza unafanya kufa kwa Yesu Kristo kwaajili ya agano Jipya kwa damu yake kuwa si kitu na kwamba utimilifu wote ulikuwa unapatikana kwa njia ya Matendo ya Sheria(Torati).

Sasa baadae ulipotimia utimilifu wa wakati, Yesu Kristo akazaliwa, Biblia inasema alizaliwa chini ya Sheria ili awakomboe walio chini ya Sheria (Wagalatia 3:4-5). Na kwa mkono wa Yesu Kristo biblia inasema ndio tulipata Neema na Kweli. Sasa hebu tuone nguvu na kazi ya Neema.

Kwanza kabisa, Neema hufundisha; Biblia inasema katika Tito 2:11-12) "Maana Neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kuukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa". Waoh! Kwangu haya ni moja ya maandiko yenye nguvu Sana. Biblia inasema kwanza, neema hii nikwaajili ya wanadamu wote, yeyote anayetaka kuingia kwenye haki ya Mungu,hilo linawezekana kabisa kwasababu Neema ipo kwaajili yake pia. Na pili inaeleza nguvu ndani ya Neema hiyo kwamba yenyewe inauwezo wa kufundisha, inafundisha watu kukataa ubaya; inakusaidia kuutambua na kuuona ubaya kisha inakupa nguvu ya kukataa ubaya huo. Na kwa kufanya hivyo Neema inakupa uwezekano wa kuishi maisha ya Kiasi, utauwa na haki muda wote utakapo kuwa hapa duniani. Mpendwa Kama hauamini kwamba watu wanaweza kuishi maisha ya haki na utauwa wakiwa duniani, basi fikiri tena, biblia inasema "….katika ulimwengu huu wa sasa".

Pili, Neema inafanya uweza wa Mungu uendelee kuwa juu ya hali zote za kibinadamu. Biblia inaonyesha kwamba Mambo yote ambayo hutoka juu huwa na nguvu kubwa sana, Neema ni moja ya Mambo hayo, inauwezo wa kuwa juu kuliko kila uovu hivyo kufanya hata dhambi za wanadamu zikiongezeka kiasi gani bado yenyewe itakuwa ndio kimbilio tosha kwa Yeyote anayetaka kusafishwa. Tusome, (Warumi 5;20-21) "Lakini Sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa Sana, na dhambi ilipozidi,Neema ilikuwa ngingi zaidi ili kwamba Kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti vivyo hivyo kwa njia ya haki, Neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana Wetu".

Tatu, Neema hutuokoa Kutoka katika Maovu na uharibifu. Ukisoma biblia sura ya Sita ya Kitabu cha Mwanzo, katika msitari wa 6 na 7. Biblia inasema watu wote walikuwa tayari wameandaliwa adhabu kuu toka kwa Bwana, Lakini Nuhu akapata Neema na kwa sababu hiyo hakuingia kwenye uharibifu.

Na Nne, Neema hutusaidia kuwa na bidii isiyoyakawaida, inayopita uwezo wa kibinadamu. Paulo kwenye kitabu cha 1Koritho 15:10 anasema "Lakini kwa Neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na Neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nilizidi Sana kufanya kazi kupita wao wote; Wala si Mimi, bali Ni Neema ya Mungu pamoja nami". Mtume Paulo anaeleza jambo la ajabu Sana hapa; kwanza, anaonyesha kwamba Kuna wakati alipokea Neema toka kwa Bwana, na baada ya kupokea Neema alikuwa anauwezo wa kufanya kazi hata kupita akina Petro na Wengine wengi na anashuhudia kabisa kwamba kwa anavyojifahamu, kazi ile haikutokana na nguvu na maarifa yake, bali Ni Neema iliyokuwa pamoja nae.

Nihitimishe kwa kusema Neema ya Mungu ya wokuvu kwa wanadamu inapatika bure kwa watu wote. Hata hivyo biblia inaonyesha kwamba huku tuko ndani ya Kristo Kuna njia za kupata Neema zaidi toka kwa Bwana la si hivyo! Tunaweza kupungukiwa neema na kusababisha uchungu mkubwa Sana katika Mwili wa Kristo. Njia za Kuongeza Neema ni pamoj na;

Kuongeza maarifa ya Neno la Mungu. Biblia inasema 2Petro 1:2 "Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana Wetu". Andiko Hilo katika Biblia ya KJV linaanza kwa kusema " May the grace and peace be multiplied unto you….. through the Knowledge of God…". Hivyo hututhibitishia kwamba Neema inaongezwa pale unapo ongeza maarifa kwa ki-Mungu.

Pia Neema huongezwa kwa njia ya Unyenyekevu. Biblia inasema 1Petro 5:5 "….Naam ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi lakini huwapa wanyenyekevu Neema".

Na mwisho kwa leo, Ni kwanjia ya Maombi, tukikaribie kiti cha Neema kwa kila wakati. Katika Waebrania 4:16 Biblia inasema "Basi na tukikaribie kiti cha Neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata Neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji". Hayo na mengine Mengi yatatufanya hata baada ya kuingia ndani ya Ufalme wa Mungu tuendelee kufanya Mambo makuu kwasababu ya kuwa na Neema ya kutosha kwenye maisha yetu ya kila siku. Kwa awamu hii ya kwanza naomba tuishie hapa na kwa Neema yake Bwana somo hili litakujia tena kwa mafunuo mengi zaidi hapo baadae. Bwana Yesu awabariki Sana.

Prepared and Written by;

Robin MWENDA

Phone; +255756814182/+255713280679

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *