SABABU ZA ROHO MTAKATIFU KUJA DUNIANI.

Yohana 14:16, 16;7

Sehemu ya Kwanza(Part 1)

Shalom! Ni matumaini yangu wewe uko salama, na unaendelea kumpenda Yesu. Baada ya kuwa tumeona angalau Kwa utangulizi Nini sababu za Yesu kuja Duniani katika Mwili, ambazo ni Pamoja na Kufanya kazi ya malipizi ya Dhambi Msalabani, kutupa uzima n.k Leo nimeona vyema tujifunze nga Kwa utangulizi kuhusu Nini hasa sababu zilizomfanya Roho Mtakatifu aje Duniani, karibu na tusafiri pamoja.

Sasa ili kuweza kufahamu vizuri kile ambacho Roho Mtakatifu alikuja kukifanya lazima tupite Kwa haraka Kwa kazi ambazo Yesu alikuwa anazifanya, utakubaliana nami kwamba Moja ya kazi kubwa aliyokuja kuifanya Yesu ilikuwa ni kurejesha ushirika kati ya Mwanadamu na Mungu na ndio Maana hata Jina lake alishatabiriwa kuwa litakuwa "Emanueli" likimaanisha Mungu pamoja na Wanadamu. Imeandikwa hivi, Isaya 7:14 "Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto wa kiume, naye atamwita jina lake Imanueli." andiko hili linarudiwa katika Agano Jipya, likionyesha kutimia Kwa unabii huo na huku linaonyesha na maana ya Neno, imeandikwa hivi, Mathayo 1:23 "Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi." Kutokana na maandiko haya mawili tunathibitisha Moja ya dhumuni kubwa kabisa la Yesu la kuja Duniani yaani kurudisha uhusiano kati ya Mungu na Wanadamu. Madhumuni mengine ni Pamoja na Kutoa uzima ili tuwe nao tele(Yohana 10:10), Kutafuta na kuokoa kile kilichopotea (Luka 19:10) na mengine Mengi.

Sasa tuingie ndani kidogo, unakumbuka hata baada ya Yesu kufanya haya yote ambayo watu sio tu walifurahia bali pia walisaidika Sana na hakika Mwokozi wao alikuwa amefika, Kuna siku aliwashangaza Sana Kwa kuwaambia kwamba ni faida kwao Yeye kuondoka… Biblia inaandika hivi, Yohana 16:7 "Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitamtuma kwenu." Yesu anawaambia Wanafunzi Jambo ambalo hawakutarajia Kanisa kulisikia ukiendelea mbele anaendelea kueleza Sababu za huyo "Msaidizi" kuja na kazi ambazo atakuwa anazifanya. Lakini mpaka hapa hebu tuone Msaidizi anayeelezwa hapa ni Nani ? Kuna maandiko mengi Saba lakini naomba nichague hili Moja Yohana 15: 26 "Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia." Aah! Mpaka hapa tunaona "Msaidizi" anayetajwa ni "Roho Mtakatifu". Sasa tuendelee; kwanini hasa Yesu anawaambia Watu wale kwamba yawafaa wao, ni faida kwao, ni bora zaidi kwao, Yeye aondoke na aje Roho Mtakatifu, na Kuna kitu anawadokeza hapa anasema Kama Yeye hataondoka basi Roho Mtakatifu hawezi kuja (hiki tutazungumza siku Nyingine), Leo tusonge mbele tu, hizi hapa binafsi naona ni moja ya sababu Muhimu zinazomfanya Yesu aseme ni bora Yeye aondoke na Roho Mtakatifu aje;

Sababu ya Kwanza, Yesu alijua kwamba Kuna njia ambayo alitakiwa kuitumia ili kukamilisha Kazi yake aliyokuja kuifanya duniani, na njia hiyo ni kujitoa mwenyewe Kama Sadaka. Biblia inasema Damu ya Mbuzi, mafahali n.k haikutosha kusafisha Dhambi(Waebrania 10:2) bali ilikuwa lazima Damu yake itolewe mara moja tu Kwa ajili ya Ulimwengu Mzima (Yohana 1:29, Isaya 53:3-5) Kwa Sababu hii alikuwa anawaandaa Wanafunzi wake na kuwahakikishia kwamba hawatakuwa peke yao.

Pili, Yesu alikuwa amefanya Kazi yake hata hivyo Kazi zake nyingi, Kubwa alizokuwa anazifanya zilisababisha mshangao mkubwa Kwa Wale walioshuhudia na wakamtukuza Mungu Kwa hizo lakini Nguvu na hamasa hiyo haikukaa ndani yao Kwa kudumu, mara nyingi ilikuwa ni Kwa Muda tu, Sasa Yesu anajua kwamba akija Roho Mtakatifu na akikaa ndani yao, hiyo nguvu itakuwa ndani yao pia milele, Kwa Mfano hebu Mtazame Petro alikuwa karibu na Yesu Muda wa kutosha, akashihudia mengi makubwa, akatembea juu ya Maji lakini bado siku ya kukamatwa Yesu alijificha. Lakini pia Yesu mwenyewe huku anawaaga Wanafunzi wake aliwatahadharisha Luka 24:49 "Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hadi mvikwe uwezo utokao juu." ooh! Kuna uwezo hawa watu walikuwa hawana bado, na tunaona wanaupata siku ya kuja Roho Mtakatifu, siku ya Pentekoste (Matendo ya Mituume 2:1-4) na

Tatu, Naona Kama wakati Yesu Yuko Duniani alikuwa anafanya kazi Kwa mipaka (Limited Jesus in functioning) hapa maana yake ni hii, utendaji wa Yesu ulizingatia zaidi uwepo wake kimwili (Physical presense), akiwa Bethinia, hayupo Yerusalemu, akiwa yudea hayupo Nazareti(zingatia hapa naongelea Yesu Mwanadamu kamili na Mungu kamili), hapa nakumbuka Mhubiri mmoja Mkongwe, nilishawahi kumsikia akisema Roho Mtakatifu ni Yesu asiye na mipaka(Unlimited Jesus). Hayo machache ndio Kwa Leo nimeona tuyatazame na yatufikirishe juu ya kauli ya Yesu ya kwamba "yawafaa ninyi Mimi niondoke…." Lakini ni Nini hasa sababu za Roho Mtakatifu kuja Duniani….basi usikose kufuatilia sehemu ya pili ya somo hili pana, zuri na lenye msaada Mkubwa Sana Kwa Kanisa Kwa nyakati zote. Bwana Yesu akubariki Sana!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *